
Hatua ya kwanza
Namna ya kuchagua solar panel itakayokufaa ni sawa kabisa na namna ya utakavyochagua battery itakayokufaa. Namna ile ile ambavyo battery kubwa itatunza umeme mwingi na kwa muda mrefu, ndivyo ilivyo hata kwa solar panel, kwamba solar panel kubwa itakusanya mionzi kutoka kwenye jua kwa muda mfupi na kwa kiasi kikubwa. Ukubwa na idadi ya solar panels utakazohitaji itategemea sana na idadi na aina ya vifaa unavyotegemea kuvitumia katika mfumo huu wa umeme jua. Vile vile itategemea ni kwa muda wa masaa mangapi utautumia umeme huu na kwamba ni kwa kipindi kirefu au kifupi kiasi gani unapata mwanga wa jua katika msimu mzima wa mwaka kwenye hilo eneo utafunga solar panels zako.
Hatua ya pili
Katika hatua hii ya pili, kuna mambo matatu unahitaji kuyazingatia wakati wa kuchagua solar panel. Unatakiwa kujua ni vifaa gani vya umeme utakuwa unatumia na vinatumia kiasi gani cha umeme kwa kila kimoja, kisha jumla ya umeme utakaoutumiwa na vifaa vyote kwa pamoja. Unapaswa kujua ukubwa na uwezo wa battery yako (wakati mwingine kufahamu hata idadi ya battery utahitaji). Ujue pia ni solar panel ya ukubwa gani (au solar panel ngapi) inayoweza kuzalisha umeme wa kutosha ili kuchaji battery kwa haraka baada ya kutumika.
Hatua ya tatu.
Fahamu ni kiasi gani cha umeme vifaa vyako vitatumia katika muda maalum ambao utatumia umeme jua. Matumizi ya umeme katika vifaa vya umeme yanasomeka katika kipimo kinachoitwa Watt(W). Kwa mfano taa yako moja (labda energy serving lamp ya 24W). Kujua nguvu ya umeme itakayotumiwa na taa hii labda kwa masaa manne(4), unatakiwa kuzidisha nguvu ya umeme inayotumiwa na taa hiyo na idadi ya masaa kwa muda wote ambao taa hiyo itawaka. Kutoka katika mfano wetu;
Chukua 24W x 4h(masaa)=96Wh
Kwa hiyo taa yako itatumia 96Wh ya umeme kwa masaa manne.
Rudia hesabu hii kwa kila kifaa chako cha umeme utakachotumia kisha jumlisha matokeo ya kila kimoja ili kupata jumla ya matumizi ya vifaa vyako vyote.
Hatua ya nne
Uwezo wa battery unapimwa kwa kipimo ambacho kitaalam kinaitwa Amp Hours(Ah). Kwa mfano battery yenye uwezo wa 17Ah, 12V. Zidisha ukubwa/uwezo wa battery na kiasi cha voltage ilichonacho. Hivyo itakuwa;
17Ah x 12V = 204Wh (kwa sababu A x V = Watt)
Yaani Current x Voltage = Power (Watt)
Kwa hiyo battery hii inaweza kuwasha taa yako hapo juu kwa masaa 204Wh/24W = 8.5h yaani masaa nane na nusu. Ikumbukwe kwamba kadri unavyotumia umeme mwingi ndivyo hata battery yako inaishiwa nguvu ya umeme upesi.
Hatua ya tano.
Ni vizuri ukajua ni kiasi gani cha umeme solar panel yako inaweza kuzalisha na kwa muda gani. Kiasi cha uwezo wa kuzalisha umeme kwa solar panel nacho kinapimwa kwa Watt(W). Kujua kiasi gani cha umeme sola yako ina uwezo wa kuzalisha ili kuchaji battery yako, unazidisha Watts za solar panel yako na idadi ya masaa solar panel yako itapokea mionzi ya jua. Matokeo utakayopata yazidishe na 0.85 (Hii inasaidia kujua kiasi sahihi cha umeme utakachopata kwani huwepo kiasi kidogo cha upotevu hutokea katika mchakato mzima wa mabadiliko kutoka nguvu ya mionzi kwenda nguvu ya umeme).
Kwa mfano solar panel ya 10W ambayo inapata mionzi ya jua kwa masaa nane(8) itakuwa hivi;
10W x 8h x 0.85 = 68Wh
Kwa hiyo solar panel hii itazalisha 68Wh kwa muda wa masaa 8.
Kwa njia hii ni rahisi kujua utahitaji solar panels na battery ngapi kwa ajili ya matumizi yako.
Ni vizuri ukafuata hatua hizi au kuomba ushauri kwa mtaalam aliyeko karibu nawe kabla ya kuamua kuzalisha umeme huu kuliko kununua tu vifaa na kumtafuta fundi akufungie. Itakugharimu siku si nyingi baada ya kuanza kutumia. Umeme jua ni aina ya umeme wa uhakika sana endapo utazingatia kanuni muhimu kuhusu aina hii ya umeme.
0 comments: