Kwa mujibu wa Tanzania D&H Survey, matumizi ya umeme mijini kwa aijli ya kupikia ni 3.8% na vijijini ni 0.2%. Wakati huo huo matumizi ya mkaa mijini kwa ajili ya kupikia ni 62% na vijijini ni 6.3%. Linapokuja suala la matumizi ya kuni hali ni mbaya zaidi kwa maeneo ya vijijini kwani watumiaji wa nishati hii inafikia 92% na mijini watumiaji wanafikia 21%.
Hizi ni takwimu za kuogopesha sana hasa kwa mazingira yetu na majaliwa ya vizazi vijavyo. Unaweza kupata picha halisi mwenyewe ni jinsi gani misitu yetu inateketea kila uchwao. Inasikitisha sana kwamba katika kila miti na misitu inayoteketetea kila mwaka ni robo yake tu ndio hupandwa tena baada ya matumizi ya ile ya awali. Hii inamaanisha misitu inazidi kuisha na itafikia wakati itabaki kuwa historia kama hatua madhubuti na za makusudi hazitachukuliwa.
Nia yangu ni kutaka kusisitiza nishati mbadala wa kuni na mkaa. Kwa wengi wetu matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia ni kama anasa kutokana na gharama kubwa ya umeme. Hata hivyo kuna nishati nyingine ya gesi ambayo wengi wetu bado hawajahamasika kabisa kuitumia. Nishati ya gesi ni rahisi sana kwa maana ya gharama kuliko hata mkaa kama utaamua kuzilinganisha. Pamoja na urahisi huo, gesi ina faida nyingi kwa mtumiaji kuliko nishati zingine zote nilizozitaja hapo juu. Jambo lingine la muhimu ni kwamba ukiondoa kuni na mkaa ambavyo vinasisitizwa kutotumiwa, usambazaji wa gesi ni rahisi sana kwa maeneo yote ya mijini na vijijini.
Hata hivyo kwa wakazi wa vijijini wana nafasi kubwa sana ya kuzalisha gesi yao wenyewe ukiachilia mbali hii gesi tunayouziwa na makampuni mbalimbali. Kuna gesi ya asili kabisa ambayo inazalishwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama na mabaki ya mimea mbalimbali. Teknolojia ya utengenezaji wa gesi hii ni rahisi na inapatikana kwa wataalamu kadhaa hapa nchini. Niliwataja wakazi wa vijijini kwa vile upatikanaji wa malighafi ya gesi hii ni mkubwa na rahisi sana vijijini. Kinachokosekana hapa ni uhamasishaji na mafunzo ya uzalishaji wa gesi ya aina hii. Kwa watu wa mijini ni vizuri wakahamasika kutumia gesi badala ya mkaa kama takwimu zinavyoonyesha hapo juu. Kufanya hivyo kutapunguza matumizi ya mkaa na kuni ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa sana kuharibu mazingira.
Ikiwa mazingira yetu yatatunzwa ipasavyo tutajihakikishia upatikanaji mzuri wa mvua ambayo itatuwezesha kuzalisha chakula cha kutosha na jambo jingine zuri ni kwa kampuni yetu ya kizalendo TANESCO kuweza kuzalisha umeme unaotokana na nguvu ya maji wa kutosha. Na hii ndio SABABU kubwa iliyonifanya leo hii nikaandika nilichokiandika. Kwamba tutunze mazingira yetu ili tupate mvua za kutosha na hivyo kuwawezesha TANESCO kuzalisha umeme wa kutosha. Hili linawezekana endapo sote kwa pamoja tutaguswa na uharibifu wa mazingira unaoendelea. Maana yake ni kwamba tubadili tabia na fikra zetu. Tufute fikra kwamba wanaoweza kutumia gesi ni matajiri tu. UKWELI ni kwamba gharama halisi za matumizi ya gesi ni ndogo kuliko gharama za kutumia mkaa. Siku nyingine MUNGU akinijaalia nitakuonesha ukweli huu kihalisia kabisa.
Sote tunafahamu kabisa kwamba TANESCO inazalisha umeme kutoka katika vyanzo kama gesi, maji na mafuta aina ya diesel kwa kiasi kidogo sana. Kwa takwimu kutoka shirika la TANESCO, uzalishaji wa umeme kutokana na gesi ni 63% na maji ni 37%. Hata hivyo kuna uzalishaji kwa njia ya maji unategemewa kuanza muda mfupi ujao ambao utazalisha jumla ya 300MW. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha umeme kitakachozalishwa ukilinganisha na vituo vingine vinavyozalisha umeme kwa njia hii. Uzalishaji huu utaongeza kiwango cha asilimia hapo juu. Ninachotaka uone hapa ni jinsi ambavyo kama tukiyatunza mazingira yetu tunaweza kupandisha kiwango kikubwa zaidi cha uzalishaji umeme wa maji kuliko ilivyooneshwa hapo juu. Kwa hivyo, njia mojawapo ya kuyatunza mazingira ni kuhamasika kutumia gesi badala ya mkaa na kuni. Vile vile tuzalishe gesi inayotokana na mabaki ya mimea na kinyesi cha wanyama pale inapobidi/wezekana.
Pamoja na hayo yote niliyoyaeleza hapo juu, bado kuna nishati nyingine mbadala tuna nafasi ya kuzizalisha. Hapa namaanisha umeme unaozalishwa kutokana na jua na upepo. Umeme wa jua unaweza kuzalishwa katika maeneo yote nchi kwani upatikanaji wa jua ni wa uhakika. Hata katika maeneo yenye mvua nyingi, baridi kali na ukungu mwingi kama vile wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Njombe mkoani Njombe, Rungwe mkoani Mbeya bado uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa matumizi ya nyumbani unawezekana. Kwa umeme unaozalishwa kutokana na upepo, tafiti zinaonesha maeneo ya Kititimo mkoani Singida na Makambako mkoani Njombe yana uwezo wa kuzalisha umeme mwingi kutokana na kasi ya upepo unaopatikana katika maeneo haya.
Wakati mwingine nitakuchambulia maeneo haya na kiasi cha umeme kinachoweza kuzalishwa. Kwa msaada wa taarifa zinazotolewa na TANESCO nitaainisha vituo vyote vinavyozalisha umeme wa gesi, maji na diesel na kiasi kinachozalishwa na vituo hivyo. Kisha tutafanya pamoja tathmini kadhaa za hali ya umeme na namna ambavyo tunaweza kuwashauri wazalishaji wa umeme namna tunavyoweza kuboresha na kuongeza upatikanaji wa umeme.
0 comments: