Sunday, 23 October 2016

NI MUHIMU KUZINGATIA HAYA



Kuna wanaosema wamo ama wanaelekea katika zama za sayansi na teknolojia halafu wapo ambao wamekuwa kwenye zama hizo kwa muda mrefu sasa. Jambo la msingi hapa ni kwamba teknolojia imekuwa ikikua kwa kasi sana. Kwa baadhi ya watu kuendana na kasi hii ya ukuaji wa teknolojia kwao sio muhimu. Hawahitaji kujifunza mambo ya msingi kabisa yahusuyo teknolojia au kujua walau kwa uchache mazao ya teknolojia.
Kwa mfano ikiwa mtu atahitaji jokofu, haoni umuhimu wowote wa kujifunza/kupata maelezo ya mtengenezaji wa jokofu hilo. Anachotaka ni kupata jokofu litakalopooza au kugandisha vyakula na vinywaji vyake. Vivyo hivyo kwa pasi, microwave, tv, n.k. Tabia au mazoea haya ni mabaya sana, ni kwa vile tu athari au hasara yake si ya moja kwa moja, yaani sio ya papo kwa hapo.

Muuzaji mmoja wa duka la vifaa/vyombo vya umeme pale Kariakoo,Dsm aliwahi kuniambia kwamba yeye hana utaalamu wowote kuhusiana na vifaa hivyo. Anasema mteja anapoingia dukani kwake na anataka kununua mfano TV anachokifanya ni kumuonesha tv za kampuni tofauti tofauti, kumjulisha bei na warranty au guarantee yake. Hivyo tu, halafu mteja anaichagua anayoitaka na wanafanya biashara. Anasema wengi wao hawahitaji kujua undani wa bidhaa wanazozitaka.
Ukweli ni kwamba Watanzania wengi tunahitaji kubadilika. Unaponunua kitu si suala la kuangalia rangi au muonekano ama urahisi wa bei tu.

Miongoni mwa mambo ya msingi sana unapotaka kununua pasi, television, jokofu, microwave, jiko la umeme, mashine ya kufulia nguo, n.k ni kuangalia kama kifaa/chombo hicho ni chenye uwezo wa kutumia umeme kidogo kwa maana ya kubana matumizi ya umeme. Ni muhimu pia kuangalia na kujua alama za ubora ikiwa zipo katika hicho kitu unachokinunua. Hata hivyo utahitaji kuwa makini sana kwani kuna alama za ubora zinazowekwa katika vifaa hivi ambazo ni 'fake'. Hili ni darasa lingine.
Ukubwa au nafasi ya kitu unachokinunua ni muhimu kuzingatiwa. Ni vizuri pia kufanya utafiti wako binafsi katika maduka mbalimbali ili kujifunza mambo ya msingi kuhusu bidhaa unayoihitaji kabla ya kuinunua. Kagua na kujiridhisha mwenyewe kama bidhaa uliyoihitaji ndio unayokabidhiwa na kama inafanya kazi vizuri. Pia kagua Receipt yako kabla ya kutoka dukani hapo ili kujua ikiwa kilichoandikwa humo ni sahihi. Jambo hili ni muhimu sana kwa siku za usoni au mara tu baada ya kufika nyumbani kifaa ulichokinunua kikaleta shida. Itunze receipt yako mahali salama. Zingatia maagizo ya warranty, hapa kumbuka kuna warranty ya mtengenezaji na muuzaji. Kumbuka kutofautisha kati ya warranty na guarantee.

Tazama, kwa mfano unanunua television mpya. Ni vizuri ukanunua flat screen LCD(Liquid Crystal Display). Hizi ni television bapa ambazo sifa yake kubwa ni kutumia umeme kidogo sana ukilinganisha na hizi tunazoziita Chogo (Cathode Ray Tube-CRT Monitor) ambazo hutumia umeme mwingi.
Epuka kununua vitu vya bei rahisi hasa hivi vinavyotumia umeme. Hapa simaanishi kila kilicho cha bei rahisi ni kibaya ila mara zote ubora wa kitu unaendana na bei yake. Ni muhimu ukajua tofauti ya 'gharama' na 'bei'. Bei inapokuwa ndogo na gharama ya kitu hicho maana yake itakuwa ndogo. Na kinyume chake ni sahihi.
Kuna watu hawawezi kuamua ikiwa watumie jiko la gesi ama la umeme. Ukweli ni kwamba jiko la umeme ni gharama kulinunua, kuliendesha na kulitunza. Hutumia nishati ya umeme nyingi ili kuivisha pishi lako. Jiko la gesi ni gharama pia kulinunua lakini hutumia nishati kidogo sana ya gesi ili kuivisha pishi lako. Mtu anayetumia gesi ana nafasi nzuri sana ya kuivisha anachokiivisha kwa haraka zaidi kwa raha kwani jiko la gesi halizalishi joto sana ukilinganisha na jiko la umeme.
Mara zote chagua bidhaa itakayodumu kwa muda mrefu. Usinunue kwa kufuata mkumbo, ni vizuri msukumo wa kununua bidhaa unayoinunua ukatokana na uhitaji ulionao kwa wakati huo.
Previous Post
Next Post

About Author

0 comments: