
Wengi wetu tumekuwa hatuna tabia au utaratibu wa kujua maana ya taarifa muhimu zilizowekwa katika bidhaa mbalimbali katika mtindo wa ALAMA au HERUFI. Leo ntakudokeza kwa kifupi maana ya herufi hizi mbili CE, nikijiegemeza zaidi kati anga la vifaa vya kielektroniki na umeme.
Kwa hapa kwetu Tanzania tuna shirika la viwango (TBS) ambalo katika bidhaa ambazo tayari imezithibitisha ubora wake huweka neno hili TZS kisha kufuatiwa na namba kadhaa mfano TZS 200.
Kwa upande wa CE ni alama ya lazima kabisa kwa bidhaa kadhaa ambazo huuzwa ndani ya Eneo la Kiuchumi la bara la Ulaya(EEA). Alama hii pia hutumika/hupatikana katika bidhaa zinazouzwa nje ya bara la Ulaya ambazo zimezalishwa au kubuniwa kwa ajili ya kuuzwa ndani ya Eneo la Kiuchumi Ulaya.
Hii ina maana kwamba kuna bidhaa nyingi ambazo zinapatikana katika nchi nyingi za bara la Afrika hususani Tanzania ambazo zina alama hii CE. Kwa hiyo utakuwa unaelewa sasa kwamba kuna bidhaa nyingi tunazipata ambazo zina hadhi ya viwango vilivyokubaliwa katika maeneo yaliyopiga hatua kubwa kimaendeleo na kiteknolojia kama bara la Ulaya. Hapa lengo langu ni kusisitiza KUANGALIA alama au herufi muhimu zinazotoa taarifa za ubora au uimara wa vifaa vya umeme unavyonunua. Ni muhimu sana. Kuna taarifa nyingine nyingi tu zinapatikana katika bidhaa tunazozinunua kila siku tu, mfano IP Code, nk. Nilichokifanya ni kukupa changamoto au kukufumbua macho kidogo tu kuhusu taarifa hizo. Unaweza kuendelea kujifunza taratibu mwenyewe kama unavutiwa kupata taarifa muhimu kuhusu kitu au bidhaa unayoitaka kabla hujainunua.
Mwisho nataka nikupe asili au kirefu cha herufi hizi CE. Ona, CE ni maneno mawili ya Kifaransa yaani Conformite Europeene. Maneno haya kwa Kiingereza ni European Conformity. Kwa tafsiri isiyo rasmi conformity ni hali au kitendo cha kufuata sheria, taratibu au viwango vilivyowekwa na jamii husika ili kutokutoka nje ya hayo waliokubaliana.
0 comments: