Monday, 3 October 2016

UNAJUA NI LINI UNAPASWA KUFANYA UKAGUZI WA MFUMO WA UMEME KATIKA JENGO LAKO?



               
Hapa jengo linajumuisha nyumba unamoishi, ofisi, duka, ghala,nk.  Kwa ujumla bila ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo hayo niliyoyataja na mengine mengi kunahatarisha usalama wetu. Wengi wetu hatujui ni lini au ni baada ya muda gani tangu majengo yetu yawekwe umeme kwa mara ya kwanza tunahitaji kuyakagua tena. Kadri utakavyoendelea kunifuatilia utafahamu polepole mambo yote haya na mengine mengi kuhusu umeme.

 Nitajitahidi kuelezea kwa lugha rahisi sana ili kila mmoja wetu aelewe. Kuna sababu nyingi za kufanya ukaguzi huu kila inapobidi, lakini sababu ya msingi sana ni usalama(Safety). Dalili kubwa ya kwanza inayoonesha jengo halikufanyiwa ukaguzi (ukiachilia mbali sababu zisizoepukika) ni pale linapotokea tatizo kubwa kama janga la moto au mtu kupigwa na umeme(electrocution). Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kunapunguza uwezekano wa majanga kama haya kutokea.
Ikiwa wewe ni mwajiri,  ni kwamba chini ya sheria za afya na usalama sehemu ya kazi (Occupational Health and Safety Act) unatakiwa kuweka mazingira salama ya mahali pa kazi kwa waajiriwa wako. Hii ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme katika maeneo yako.
Baadhi ya vitu vinavyotakiwa kukaguliwa ni pamoja na vifaa vyote vinavyotumia umeme, swichi za kuwashia taa, swichi za ukutani, swichi kuu, waya zilizotumika, kikata umeme(circuit breaker), mfumo wa earth, n.k. Kumbuka: Ili kufanya ukaguzi ulio makini na unaozingatia taalumaya umeme, fundi atalazimika kuzima umeme katika jengo lako wakati fulani na atahitaji kuyafikia maeneo yote ya nyumba yako(sio baadhi).

Ukaguzi wa mifumo ya umeme kutokana na mazingira yetu unapaswa  kufanyika;
Ø      Wakati nyumba /jengo lina zaidi ya miaka kumi(10) tangu lilipofungwa umeme  kwa mara ya kwanza.
Ø     Wakati unanunua nyumba/jengo jipya.
Ø     Wakati umefanya ukarabati mkubwa katika nyumba/jengo lako.
Ø    Wakati unaongeza vifaa vingine vinavyotumia umeme ambavyo awali  havikuwepo.
Ø     Wakati unagundua kwamba matatizo ya umeme yanajirudia mara kwa mara  katika nyumba/jengo lako.
Ø     Au wakati unagundua kwamba matumizi ya umeme ni makubwa(malipo ni  makubwa) kuliko uhalisia.
Ø     Na wakati mwingine kikata umeme(Circuit Breaker) inapokuwa inakata umeme  mara kwa mara.

Ikiwa una maswali au dukuduku lolote tumia email yangu kabukaasa@gmail.com nitajibu maswali yako.
Nitaendelea pia kukuletea mambo mengi ambayo nimegundua wengi hawajui ingawa ni madogo madogo na muhimu kwao. Ni mambo ambayo huhitaji kwenda darasani ila unahitaji ufafanuzi na maelezo kiasi kutoka kwa mtaalam. Kesho ntakueleza namna ya kuchagua jokofu linalokufaa.                                            

                                                    
Previous Post
First

About Author

0 comments: