KWA NINI UMEME NI HATARI
Kuna sababu nyingi sana zinazonipa ujasiri wa kukutahadharisha na kukuambia umeme ni hatari. Ni hatari sana kwa maisha yako endapo tu hutazingatia kanuni zake. Hata hivyo hatuna namna ya kukwepa kutotumia umeme katika zama hizi za mageuzi makubwa ya teknolojia. Ukiweka pembeni madhara ya umeme kwa vifaa vinavyotumia umeme na mazingira kwa ujumla, umeme una madhara makubwa sana kwa mwili wa binadamu. Umeme huu tunaofurahia kuutumia una uwezo wa kuuunguza mwili, kujeruhi mishipa ya fahamu, kusababisha kifo au kuzimia.
Wataalamu wa viumbe hai wanasema kwa kiasi kikubwa mwili wa binadamu umejawa na maji. Hali hii inasabaisha umeme kupita katika mwili wa binadamu bila kipingamizi kwa kiasi kikubwa. Madhara au majeraha yanayosababishwa na umeme katika mwili hutofautiana kutokana na udogo au wingi wa kiasi cha umeme uliopita hapo pamoja na urefu au ufupi wa muda umeme umepita katika mwili huo. Kiasi kidogo tu cha 1mA ambayo ni sawa na 0.001A kinaweza kumfanya mtu ajisikie vibaya na kuhisi maumivu kama vile anachomwachomwa na visindano vidogo vidogo.
Hata hivyo, kadri kiwango cha umeme kinavyoongezeka ndivyo mshituko na maumivu makali yanavyoongezeka au kuwa makubwa katika mwili wa binadamu. Hali hii husababisha pia misuli kukakamaa na kuathiri viungo vingine vya mwili ikiwa ni pamoja na kuathiri utendaji kazi wa kawaida wa moyo na mapafu. Wakati mwingine nitakuelezea namna bora ya kujikinga na hatari za umeme.
Tags:
0 comments: