Sunday, 6 November 2016

UTATA KUHUSU RADI MIONGONI MWA JAMII YETU NA MADHARA YAKE


Wengi wenu mtakubaliana na mimi kwamba maana halisi ya radi imekuwa ikipotoshwa sana katika jamii zetu hapa nchini. Nakumbuka nikiwa mtoto niliambiwa radi ni mnyama aina ya kondoo, wengine waliambiwa radi ni mnyama asiyefahamika mwenye miguu sita. Mke wangu anasema aliambiwa radi ni matokeao ya mgongano wa mapipa yaliyo angani. Na kila mtu angeweza kutoa maana tofauti tofauti juu ufahamu alionao kuhusu radi.

Kwa kifupi sana, katika umeme tunasema radi ni matokeo ya mgongano wa mawingu yenye chaji tofauti za umeme yaani hasi na chanya. Wengi tunajua kwamba sehemu ya juu ya wingu huwa na chaji chanya na sehemu yake ya chini ni hasi. Kumbuka ardhi ina chaji chanya. Mgongano huu wa mawingu hutokea baada ya mawingu kupoteza hali yake ya utulivu kutokana na kuongezeka kwa joto la tabaka la chini kabisa la mawingu na unyevunyevu mwingi kutoka ardhini. Au mara chache hutokana na ongezeko la hali ya baridi katika tabaka la juu kabisa la mawingu. Ndio maana mara nyingi radi hutokea wakati wa mchana na mara chache sana wakati wa usiku. Na kwa sababu lazima kuwepo na unyevunyevu radi mara zote hutokea wakati mvua ikinyesha. Isipokuwa kwa wenzetu wa Sumbawanga ambao inasemekana radi hutokea pia wakati wa mchana kweupe, jua kali na hakuna mvua(ninatania lakini).

Chaji hizi  tofauti ni lazima ziwe kubwa kwa maana ya kiasi ili kuweza kupenya katika hewa kati yao na kuzalisha umeme. Hii ni kwa sababu hewa ina ukinzani mkubwa sana kwa umeme. Ikumbukwe kwamba mgongano mmoja tu kati ya mawingu unaweza kuzalisha umeme mwingi wa hadi milioni 100V.  Huu ni umeme mkubwa sana ukizingatia kwamba kwa matumizi ya nyumbani tunahitaji kiasi cha 220/230V. Mgongano huu huzalisha joto na mwanga mkali sana. Bahati nzuri ni kwamba huisha na kufifia mapema sana.

Kwa hiyo RADI ni UMEME. Ni umeme mkubwa unaoambatana na mwanga mkali na sauti kubwa sana. Kwa sababu ni umeme mkubwa, mara zote husababisha madhara makubwa sana kwa binadamu na mazingira yake. Madhara kwa binadamu ni pamoja na kifo au majeraha na hasara inayotokana na uharibifu wa mali. Lakini radi huharibu miundombinu ya umeme, mimea na nyumba pia. Kwa kiasi kikubwa madhara ya umeme yanaweza kuepukika kama kila mmoja ataelimishwa na kufuata taratibu za kujikinga na madhara yake. Kwa wenye majengo marefu wanahitaji kufunga kifaa kinachoitwa Lightening arrestor au thunderstorm arrestor. Katika majengo ya kawaida ni muhimu kuhakikisha Earthing System (Grounding) iko vizuri. Hakikisha wakati mvua inanyesha umevaa viatu au kandambili zenye soli pana kiasi cha kutosha. Ikiwezekana zima kabisa umeme unapoona dalili za radi, unaweza kuacha taa tu zinawaka ikiwa kutakuwa na giza wakati huo. Kamwe usisimame au kukaa katika maji au kusimama chini ya nguzo, mti mbichi au kitu chochote kinachokuzidi urefu na kina uwezo wa kupitisha umeme. Mara zote radi hutafuta njia fupi na rahisi ili kukamilisha muunganiko wake na ardhi.

Maeneo mengi ya vijijini watu wanapokutwa na mvua na hakuna sehemu ya kujikinga na mvua, hukimbilia chini ya miti. Ni hatari sana kufanya hivyo kwa sababu ikiwa mti uliosimama chini yake utakuwa ndio mrefu kuliko kitu kingine chochote kinachopitisha umeme mahali hapo, basi radi itakamilisha muunganiko wake na ardhi kupitia mti huo na hapo ndipo utakapokutana na balaa kubwa la kifo ama majeraha makubwa. Lakini pia kunapokuwa na dalili za radi jizuie kutembea kwa mwendo mrefu katika sehemu ya wazi sana ambayo wewe ndio utakuwa na kimo kirefu kuliko kitu kingine. Vinginevyo unaweza kuishia kuwa mkaa.

Previous Post
Next Post

About Author

0 comments: