Usafirishaji wa umeme kwa kutumia nyaya zilizopita juu(yaani nguzo) sio tu ni hatari kwa mfumo wenyewe bali kwa maisha ya watu na mali zao. Naomba nieleweke wazi kwamba simaanishi mfumo huu haufai kabisa ila ukilinganisha na mfumo wa kusafirisha umeme kwa nyaya zilizopita chini ya ardhi, utagundua kwamba njia ya nyaya za umeme chini ya ardhi ni salama na uhakika zaidi.
Sote tunafahamu namna ambavyo kunakuwa na hitilafu za mara kwa mara kwenye mifumo ya umeme nyakati za mvua nyingi. Hitilafu hizi zingeweza kuepukika au kupungua sana endapo mfumo wa kupitisha ardhini nyaya za kusafirisha umeme ungetumika. Ikumbukwe kwamba mara nyingi katika maeneo yetu mengi(sio yote) mvua kubwa huambatana na upepo mkali. Upepo huo huathiri uimara wa mifumo ya kusafirishia umeme. Vile vile mvua hizi huambatana na radi ambayo ni adui mkubwa sana wa umeme na mifumo yake(ingawa radi ni umeme ila katika hali ambayo ni tofauti na umeme wa kawaida tuliouzoea).
KUMBUKA, nia ya makala hii sio kuelezea aina ya njia za kusafirishia umeme. LENGO langu ni kutaka wewe msomaji wangu ujue na kuelewa mambo ya kuzingatia na namna ya kujikinga na athari zitokanazo na madhara ya mvua na upepo kwenye mifumo ya umeme kwa ujumla wake. Ni vizuri ikiwa utazingatia yafuatayo;
- Hakikisha mfumo wa umeme katika nyumba, ofisi au jengo lolote una Earthing(Grounding) System nzuri.
- Ikiwa mvua inayonyesha inaambatana na radi au upepo mkali, nashauri uzime vifaa vyote vinavyotumia umeme hasa vile ambavyo ni rahisi kuathiriwa na radi mfano TV, radio, jokofu, jiko la umeme, nk.
- Hakikisha nyayo zako hazina muunganiko wa moja kwa moja na ardhi. Maana rahisi ni kuvaa kiatu ama kandambili mvua iliyoambatana na radi inaponyesha. Sambamba na hili kaa mbali na maji yoyote yaliyozagaa ardhini.
- Zima kabisa simu yako ya mkononi mpaka radi itakapokoma.
- Usichaji simu wakati wa mvua ya namna hii.
- Ikiwa umeme utakatika kutokana na athari za mvua, zima switch socket zote. Ikiwezekana chomoa plug zote kutoka kwenye switch socket.
- Kama circuit breaker itakuwa imejizima wakati wa mvua kubwa, tafadhali wasiliana na mtaalam wa umeme unayemwamini kabla ya kuamua kuiwasha tena.
- Usitoke nje bila sababu ya msingi mvua inapoendelea kunyesha.
- Usiguse waya, mti, nguzo au chuma chochote ambacho kimeanguka ardhini kutokana na mvua au upepo.
- Toa taarifa TANESCO kwa uharibifu wowote uliotokea kwenye miundombinu ya kusafirishia umeme.
- Ikiwa nyaya za umeme karibu yako zimezongwa na miti au matawi yake, toa taarifa TANESCO kabla ya kuamua kukata au kuyapunguza.
- Hakikisha una namba ya simu ya dharura ya TANESCO ya eneo husika.
- Jiridhishe walau mara moja kwa mwezi kujua kama circuit breaker yako ni nzima na inafanya kazi ipasavyo. Ni rahisi tu, angalia circuit breaker usawa wa macho yako kuna kitufe cha rangi ya njano, damu ya mzee, ama rangi nyingine yeyote. Kitufe hicho kina alama ya herufi "T" bonyeza hapo mara moja. Ikiwa circuit breaker itajizima basi ujue ni nzima na kinyume chake ni mbovu.
Earth wire ina kazi gani ktk umeme
ReplyDeleteSwala erath wire ni nyutro au
ReplyDeleteNaelewa vizur kabisa kupitia hii page, hadi naona somo linakuwa fupi... Hongera saana
ReplyDelete