Katika hali ya kawaida kabisa, wengi wetu tunafahamu au tumesikia kuhusu umeme unaopatikana kutokana na nishati inayokusanywa kutoka juani. Wakati fulani niliwahi kuandika humu kuhusu uzalishaji wa umeme jua. Vyanzo vikubwa vya uzalishaji wa umeme hapa kwetu Tanzania ni maji, gesi asilia, diesel na jua. Kuna vyanzo vingine kama upepo, makaa ya mawe, mabaki ya miti, miwa, n.k ambavyo havitumiwi sana pengine kutokana na ugumu wake katika kuzalisha umeme.
Ninachokiona hapa ni kutokuwepo kwa uhamasishaji wa kutosha wa kuzalisha na kutumia umeme huu. Kwa kiwango cha upeo wangu, naamini kabisa kuzalisha umeme wa jua ni njia rahisi kuliko zote nilizozitaja hapo juu. Hapa nawalenga zaidi watumiaji wadogo wa umeme. Nasema ni rahisi kwa sababu ya upatikanaji rahisi wa vifaa vya kuzalishia umeme wa aina hii na teknolojia nyepesi inayotumika katika ufungaji wa vifaa vyake. Jambo zuri zaidi ni uwepo wa wataalam wa kutosha wenye ujuzi wa umeme jua katika jamii zetu.
Ni kweli kwamba si serikali pekee yenye wajibu wa kuhamasisha hili, lakini naamini serikali ina nafasi zaidi. Tunahitaji kuhamasishana wenyewe na kuwa na mitazamo ya kutafuta njia rahisi za kujikwamua katika matatizo yanayotukabili. Katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na kukosekana kwa umeme wa kutosha ama wa uhakika, njia ya kwanza kabisa ambayo ni rahisi na wengi wetu tunaweza kuimudu ni kwa kuzalisha umeme jua. Wengi wamekuwa wakiulalamikia umeme jua kwamba sio wa uhakika, lakini ukweli ni kwamba umeme huu ni wa uhakika. Tatizo ni kwamba wengi waliothubutu kuzalisha umeme huu hawakupata ushauri mzuri wa namna ya kununua vifaa na kuunganisha kitaalam kutokana na matumizi yao.
Kwa bahati nzuri umeme huu unaweza kuzalishwa katika maeneo yote ya Tanzania. Labda sehemu chache kadhaa za maeneo ya Mufindi mkoani Iringa na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Njombe na Makete mkoani Njombe ambayo pengine yanaweza kukosa jua la kutosha katika miezi miwili au mitatu ya mwaka.
0 comments: