Tuesday, 26 December 2017

MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUJIKINGA NA ATHARI ZA UMEME ZINAZOSABABISHWA NA MVUA KUBWA INAYOAMBATANA NA RADI PAMOJA NA UPEPO MKALI




Usafirishaji wa umeme kwa kutumia nyaya zilizopita  juu(yaani nguzo) sio tu ni hatari kwa mfumo wenyewe bali kwa maisha ya watu na mali zao. Naomba nieleweke wazi kwamba simaanishi mfumo huu haufai kabisa ila ukilinganisha na mfumo wa kusafirisha umeme kwa nyaya zilizopita chini ya ardhi, utagundua kwamba njia ya nyaya za umeme chini ya ardhi ni salama na uhakika zaidi.

Sote tunafahamu namna ambavyo kunakuwa na hitilafu za mara kwa mara kwenye mifumo ya umeme nyakati za mvua nyingi. Hitilafu hizi zingeweza kuepukika au kupungua sana endapo mfumo wa kupitisha ardhini nyaya za kusafirisha umeme ungetumika. Ikumbukwe kwamba mara nyingi katika maeneo yetu mengi(sio yote) mvua kubwa huambatana na upepo mkali. Upepo huo huathiri uimara wa mifumo ya kusafirishia umeme. Vile vile mvua hizi huambatana na radi ambayo ni adui mkubwa sana wa umeme na mifumo yake(ingawa radi ni umeme ila katika hali ambayo ni tofauti na umeme wa kawaida tuliouzoea).

KUMBUKA, nia ya makala hii sio kuelezea aina ya njia za kusafirishia umeme. LENGO langu ni kutaka wewe msomaji wangu ujue na kuelewa mambo ya kuzingatia na namna ya kujikinga na athari zitokanazo na madhara ya mvua na upepo kwenye mifumo ya umeme kwa ujumla wake. Ni vizuri ikiwa utazingatia yafuatayo;
  1. Hakikisha mfumo wa umeme katika nyumba, ofisi au jengo lolote una Earthing(Grounding) System nzuri.
  2. Ikiwa mvua inayonyesha inaambatana na radi au upepo mkali, nashauri uzime vifaa vyote vinavyotumia umeme hasa vile ambavyo ni rahisi kuathiriwa na radi mfano TV, radio, jokofu, jiko la umeme, nk.
  3. Hakikisha nyayo zako hazina muunganiko wa moja kwa moja na ardhi. Maana rahisi ni kuvaa kiatu ama kandambili mvua iliyoambatana na radi inaponyesha. Sambamba na hili kaa mbali na maji yoyote yaliyozagaa ardhini.
  4. Zima kabisa simu yako ya mkononi mpaka radi itakapokoma.
  5. Usichaji simu wakati wa mvua ya namna hii.
  6. Ikiwa umeme utakatika kutokana na athari za mvua, zima switch socket zote. Ikiwezekana chomoa plug zote kutoka kwenye switch socket.
  7. Kama circuit breaker itakuwa imejizima wakati wa mvua kubwa, tafadhali wasiliana na mtaalam wa umeme unayemwamini kabla ya kuamua kuiwasha tena.
  8. Usitoke nje bila sababu ya msingi mvua inapoendelea kunyesha.
  9. Usiguse waya, mti, nguzo au chuma chochote ambacho kimeanguka ardhini kutokana na mvua au upepo.
  10. Toa taarifa TANESCO kwa uharibifu wowote uliotokea  kwenye miundombinu ya kusafirishia umeme.
  11. Ikiwa nyaya za umeme karibu yako zimezongwa na miti au matawi yake, toa taarifa TANESCO kabla ya kuamua kukata au kuyapunguza.
  12. Hakikisha una namba ya simu ya dharura ya TANESCO ya eneo husika.
  13. Jiridhishe walau mara moja kwa mwezi kujua kama circuit breaker yako ni nzima na inafanya kazi ipasavyo. Ni rahisi tu, angalia circuit breaker usawa wa macho yako kuna kitufe cha rangi ya njano, damu ya mzee, ama rangi nyingine yeyote. Kitufe hicho kina alama ya herufi "T" bonyeza hapo mara moja. Ikiwa circuit breaker itajizima basi ujue ni nzima na kinyume chake ni mbovu.



Friday, 14 April 2017

IJUE TOFAUTI KATI YA VOLTAGE, CURRENT NA RESISTANCE.

Walio wengi wamekuwa wakichanganya maana hasa ya voltage na current. Katika vifaa vingi vinavyotumia umeme majumbani mwetu ni kawaida kuona maelezo kadhaa. Kwa mfano utaona 220V, 50H, 2A, 100W, n.k. Haya ni maelezo muhimu unayopaswa kuyafahamu japo kwa kiasi kidogo.

Nchi ya kwetu inatumia umeme ulio katika kiwango cha 220V, inaweza kufikia 240V. Nchi zingine kama Marekani na zingine zinatumia umeme ulio katika kiwango cha 110V. Ni muhimu kujua mambo haya. Tukumbuke kwamba naongelea umeme ulio katika mfumo wa line moja (Single Phase  System), yaani waya mmoja wa live na ule wa neutral.

50Hz inaonesha frequency inayokubalika katika nchi yetu. Kwa nchi nyingine hasa zinazotumia 110V utagundua wa frequency yao ni 60Hz. Sina uhakika kama kuna maneno rasmi ya kiswahili kwa maneno haya Voltage na Current.
Resistance kwa kiswahili kisicho rasmi ni Ukinzani. Unaweza kutengeneza akilini mwako picha ya bomba linalopitisha maji yanayosukumwa na pampu ya maji. Ile Pressure ya maji ndio Voltage kwenye umeme, kile Kiasi cha Maji kwenye bomba ndio Current. Kwa kifupi kabisa nafikiri unaweza ukawa umepata picha ya maana rahisi ya voltage na current. Ukinzani ambao maji yanakutana nao wakati yakisukumwa ndani ya bomba ni sawa na Resistance katika umeme.

Kipimo cha current ni Ampere(A), voltage ni Volt(V) na resistance ni Ohm. Kwa uelewa zaidi angalia picha niliyoiambatisha na maelezo hayo.

Thursday, 13 April 2017

SERIKALI IWEKE MSISITIZO KWENYE UZALISHAJI WA UMEME JUA KWA MATUMIZI YA NYUMBANI NA OFISINI

SERIKALI IWEKE MSISITIZO KWENYE UZALISHAJI WA UMEME JUA KWA MATUMIZI YA NYUMBANI NA OFISINI

Katika hali ya kawaida kabisa, wengi wetu tunafahamu au tumesikia kuhusu umeme unaopatikana kutokana na nishati inayokusanywa kutoka juani. Wakati fulani niliwahi kuandika humu kuhusu uzalishaji wa umeme jua. Vyanzo vikubwa vya uzalishaji wa umeme hapa kwetu Tanzania ni maji, gesi asilia, diesel na jua. Kuna vyanzo vingine kama upepo, makaa ya mawe, mabaki ya miti, miwa, n.k ambavyo havitumiwi sana pengine kutokana na ugumu wake katika kuzalisha umeme.

Ninachokiona hapa ni kutokuwepo kwa uhamasishaji wa kutosha wa kuzalisha na kutumia umeme huu. Kwa kiwango cha upeo wangu, naamini kabisa kuzalisha umeme wa jua ni njia rahisi kuliko zote nilizozitaja hapo juu. Hapa nawalenga zaidi watumiaji wadogo wa umeme. Nasema ni rahisi kwa sababu ya upatikanaji rahisi wa vifaa vya kuzalishia umeme wa aina hii na teknolojia nyepesi inayotumika katika ufungaji wa vifaa vyake. Jambo zuri zaidi ni uwepo wa wataalam wa kutosha wenye ujuzi wa umeme jua katika jamii zetu.

Ni kweli kwamba si serikali pekee yenye wajibu wa kuhamasisha hili, lakini naamini serikali ina nafasi zaidi. Tunahitaji kuhamasishana wenyewe na kuwa na mitazamo ya kutafuta njia rahisi za kujikwamua katika matatizo yanayotukabili. Katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na kukosekana kwa umeme wa kutosha ama wa uhakika, njia ya kwanza kabisa ambayo ni rahisi na wengi wetu tunaweza kuimudu ni kwa kuzalisha umeme jua. Wengi wamekuwa wakiulalamikia umeme jua kwamba sio wa uhakika, lakini ukweli ni kwamba umeme huu ni wa uhakika. Tatizo ni kwamba wengi waliothubutu kuzalisha umeme huu hawakupata ushauri mzuri wa namna ya kununua vifaa na kuunganisha kitaalam kutokana na matumizi yao.

Kwa bahati nzuri umeme huu unaweza kuzalishwa katika maeneo yote ya Tanzania. Labda sehemu chache kadhaa za maeneo ya Mufindi mkoani Iringa na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Njombe na Makete mkoani Njombe ambayo pengine yanaweza kukosa jua la kutosha katika miezi miwili au mitatu ya mwaka.

Tuesday, 7 February 2017

AUTOMATIC VOLTAGE REGULATOR (AVR)



Ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba wengi wetu hatufahamu AVR ni nini. Kwa sababu hiyo hata umuhimu wa kifaa hiki haufahamiki. Kwa wale wanaojua umuhimu wake ni kawaida kabisa kuona zaidi ya AVR moja katika nyumba ama ofisi zao. Kwa sababu ya umuhimu wake sio ajabu kuona AVR sebuleni, chumbani au jikoni ikihudumia vifaa vinavyohitaji huduma yake.

Hata hivyo si vifaa vyote vya majumbani au ofisini vinahitaji kuunganishwa na AVR. Mfano wa vifaa hivyo ni feni, blower, jiko la umeme, pasi, n.k. Najua una shauku ya kujua ni vifaa gani vitahitaji kuunganishwa na AVR na kwamba kwa nini vifaa hivyo viunganishwe na kifaa hiki muhimu. Nitakutajia vifaa baadhi kama TV set, computer, jokofu(fridge), kingamuzi, music system, n.k. Ni muhimu vifaa hivi vikaunganishwa na AVR kutokana na unyeti na urahisi wa kuathiriwa kwa mifumo yake kunapotokea kiasi cha umeme kisichokubalika kuingia katika mifumo yake.

Automatic Voltage Regulator (AVR) ni kifaa chenye mchanganyiko wa umeme na mifumo ya kielektroniki kinachofanya kazi ya kuhakikisha umeme unaotoka kuelekea kwenye chombo chako cha umeme unakuwa wa uhakika na katika kiwango sahihi kinachotakiwa. AVR zinapatikana katika ukubwa tofauti tofauti. Ninaposema ukubwa namaanisha uwezo wake wa kupokea na kutoa kiasi cha umeme unaohitajika. Kwa hiyo maana yake ni kwamba kabla ya kununua AVR yako ni muhimu sana kujua idadi na kiasi cha umeme ya kila kifaa chako unachokusudia kukiunganisha kwenye AVR. Uwezo wa AVR unapimwa na kipimo ambacho kitaalamu kinaitwa VA. Kwa hiyo kuna AVR za ukubwa wa 500VA, 1000VA, 1500VA, 2000VA, 3000VA, 5000VA. VA ni matokeo ya Voltage x Ampere. Kwa wale waliofanikiwa kusom Physics kidogo wataelewa kwamba VA inamaanisha Power, ingawa katika umeme kuna aina nyingi za power. Sijakusudia kuongelea power ila nilitaka ujue kwamba hizo tarakimu hapo juu zinawakilisha Power (Nguvu/uwezo wa umeme).

Ni muhimu sana kutumia AVR nyumbani au ofisini kwako kwa sababu umeme unaoingia katika majengo yetu ni  wakati fulani unacheza cheza. Yaani unapanda na kushuka (unaongezeka na kupungua).  Hali ya namna hii ya umeme inaweza kusababishwa na radi, mifumo mibovu au iliyochoka ya kudhibiti mwenendo wa umeme na wakati fulani uharibifu wa dharura wa mifumo ya kusafirisha umeme. Kumbuka nimesema wakati fulani, namaanisha si mara zote hali hii hutokea, ni mara chache sana. Sasa hali hii ya kupanda na kushuka kwa umeme inaweza kusababisha  vifaa/vyombo vyako vya umeme kupata uharibifu kama sio kuviangamiza kabisa.

AVR ina mfumo mzuri ndani yake wa kukinga na kulinda vifaa vyako vya umeme wakati wote. Tatizo likiwa kubwa zaidi AVR inauzuia kabisa umeme kuingia katika kifaa chako. Hivyo ni bora kuingia gharama ya kuwa na AVR nyumbani au ofisini kwako.


Tuesday, 15 November 2016

GROUNDING(EARTHING) NI NINI?



Kwa kawaida kama ilivyo kwa binadamu, umeme unataka kupita katika njia fupi na rahisi kupitika. Umeme hupita katika njia iliyo rahisi kwake kurudi ardhini. Njia pekee inayotumiwa na umeme kurudi ardhini bila madhara yote ni kupitia katika waya ambao kwa lugha ya kiingereza unaitwa Earth Wire na kisha Earth Rod.  Mchakato mzima wa kukamilisha ufanyaji kazi wa huu mfumo unaitwa Grounding. Ikiwa kutatokea tatizo katika waya unaobeba umeme baada ya matumizi(neutral wire), au tatizo lolote la kiufundi ambalo litasababisha ongezeko la ghafla la umeme kutokana na radi kwa mfano, basi earth wire itaubeba umeme huu wa ziada kwenda ardhini. Kwa muunganiko huu wa earth wire na earth rod, ardhi inafikika kirahisi sana na umeme. Maana yake ni kwamba mfumo huu wa grounding una wajibu wa kumlinda mtumiaji wa umeme inapotokea tatizo la umeme.

Ikiwa radi ingepiga katika nyumba yako ingeweza kusababisha hatari katika mfumo wako wa umeme na madhara mengine(Soma kuhusu radi katika somo lililotangulia). Lakini kama mfumo huo umeunganishwa ipasavyo na mfumo wa earth(Grounding) kiasi chote cha umeme wenye madhara kwa mtumiaji au vifaa vya umeme kitaishia ardhini badala ya kuunguza kila kitu kilichounganishwa katika umeme kwa wakati huo au kumdhuru binadamu.

Sote tunafahamu kwamba ardhi ni kipitisha umeme kizuri kwa asili yake. Na kama nilivyosema awali umeme unapenda kupita katika njia rahisi na fupi, kwa hivyo ku-ground mfumo wako wa umeme ni kuufanya umeme wenye madhara kwako kupata mahali pa kupita kwa urahisi badala ya kwenda ardhini kupitia mwili wako. Hivyo kwa kifupi kabisa, Earthing au Grounding ni kuunganisha vifaa vyako vinavyotumia umeme katika ardhi ya dunia kwa kutumia waya(Earth wire) na fimbo(Earth rod) mara nyingi ya shaba ambayo huzikwa katika ardhi yenye unyevu wa kutosha.

Wednesday, 9 November 2016

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPONUNUA BULB KWA MATUMIZI YA NYUMBANI




Katika hali ya kawaida kabisa sitegemei mtu atamtafuta fundi umeme inapotokea taa imeungua katika chumba, ofisi au nyumba yake. Kwa yeyote yule, taa isipowaka jambo la kwanza atakalofikiri ni taa kuungua. Mara nyingi ukweli huwa ni huo isipokuwa labda kama imetokea ni idadi fulani ya taa haziwaki na kwamba tatizo hili limeanza kwa muda mmoja basi huwa kuna sababu zingine za kiufundi. Nataka kutoa ushauri kwako kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia unapoamua kununua bulb mpya.

Kutokana na ongezeko la aina tofauti tofauti ya taa zinazotumia umeme, ni ukweli kwamba kumetokea machaguo mengi ya kutosha ya taa hizi.  Ni vizuri ukazijua aina mbalimbali ya taa zinazotumia umeme kidogo. Pamoja na kuwepo aina nyingi sana ya bulb, leo ntaongelea aina mbili tu ambazo ndizo za kileo na zinatumia umeme kidogo kama ambavyo umeziona katika picha hapo juu mapema. Kuna Compact Fluorescent Light(CFL) ambazo wengi tumezoea kuziita Energy Savor na Light Emitting Diode(LED) ambazo kwa hapa Tanzania wengi huzitumia sana katika umeme wa mfumo jua (Solar Power) na kwenye Tochi nyingi sana za siku hizi.

Bulb za kawaida (Incandescent bulb) ambazo zilizoeleka kwa miaka mingi, kwa sasa wengi hawazitumii kabisa ingawa bado zinapatikana madukani. Imekubaliwa na wataalam duniani kwamba taa za ina hii zisitengenezwe tena ila zilizokuwa tayari zimetengenezwa ziuzwe mpaka pale zitakapoisha. Taa hizi zinapatikana katika ukubwa wa 100W, 80W, 60W na 40W. CFL na LED zinatumia umeme kidogo sana japo nazo zinazidiana. Hapa chini nakuonesha kiasi cha umeme kila aina ya taa inatumia kwa kiasi kile kile cha mwanga inachotoa.

Bulb ya kawaida            CFL(Energy Savor)              LED
         100W                              20W                            18W      
           60W                              12W                            10W
           40W                               9W                               6W


  1. Ijue aina ya bulb fitting unayotumia. Hapa namaanisha ujue aina ya mahali unapofunga au kuchomeka taa yako. Kuna bulb fitting za pin na screws yaani za kuchomeka taa au kuiweka kwa mtindo wa kuzungusha kwa maana ya kufunga. Kama huwezi kutofautisha aina hizi ni vizuri ukachukua taa iliyoungua na kwenda nayo katika duka unalotaka kununua.
  2. Kama nilivyosema awali, kuna aina nyingi ya bulb kwa sasa. Usiogope kununua Energy savor au LED kwa sababu ya ughali wa bei yake, kununua bulb za aina hii kutaokoa gharama kubwa sana kama nilivvoonesha tofauti ya matumizi yake ya umeme hapo juu. Faida kubwa zaidi ni kwamba taa hizi hudumu kwa muda mrefu sana ukilinganisha na hizi za kawaida.
  3. Tambua rangi na ukubwa wa mwanga unaohitaji. Maana yake ujue ni taa ya Watts(W) ngapi unaitaka, usinunue tu ili mradi umepata taa mpya. Mwanga unaohitaji utategemea na ukubwa wa chumba na matumizi ya chumba chenyewe. Kadri chumba kinavyokuwa kikubwa kitahitaji taa yenye mwanga mkubwa zaidi. Ni vzr ukajua pia kwamba kadri Watts zinavyoongezeka ndivyo  mwanga unakuwa mkubwa.
  4. Tafuta taa yenye umbo na muonekano mzuri. Wengi wanaweza kubeza hili, Ukweli ni kwamba kila aina ya umbo ina namna yake ya kusambaza umeme katika chumba. Angalia maumbo tofauti ya bulb niliyoonesha hapo juu. Hata hivyo muonekano mzuri wa bulb hupendezesha pale ilipo. Aina ya umbo hutegemea pia mahali kitanda kilipo kwa chumbani au mpangilio wa meza na viti sebuleni.
  5. Nunua taa yenye viwango unavyohitaji. Bulb iliyokidhi viwango itadumu kwa muda mrefu, hutoa mwanga wake haraka mara baada ya kuwashwa, haizalishi joto na haipotezi uwezo wake kutokana na kutumika kwa muda mrefu. Angalia taa itakayotumia umeme kidogo kutoa mwanga wa kutosha.
  6. Nunua taa kulingana na matumizi ya chumba au jengo. Ikiwa ni ghala huwezi kununua taa kama unayotumia sebuleni, au chooni ukanunua taa kama unayotumia chumbani. Huhitaji taa ya mwanga mkali chooni, bafuni au stoo. Ikiwa ni chumba cha kusomea bila shaka utahitaji taa yenye mwanga wa wastani ambao sio mdogo wala sio mkali sana. Ikiwa utakuwa katika mwanga unaoumiza macho yako ni vizuri ukaomba ushauri au ukabadilisha taa mwenyewe.


Sunday, 6 November 2016

UTATA KUHUSU RADI MIONGONI MWA JAMII YETU NA MADHARA YAKE


Wengi wenu mtakubaliana na mimi kwamba maana halisi ya radi imekuwa ikipotoshwa sana katika jamii zetu hapa nchini. Nakumbuka nikiwa mtoto niliambiwa radi ni mnyama aina ya kondoo, wengine waliambiwa radi ni mnyama asiyefahamika mwenye miguu sita. Mke wangu anasema aliambiwa radi ni matokeao ya mgongano wa mapipa yaliyo angani. Na kila mtu angeweza kutoa maana tofauti tofauti juu ufahamu alionao kuhusu radi.

Kwa kifupi sana, katika umeme tunasema radi ni matokeo ya mgongano wa mawingu yenye chaji tofauti za umeme yaani hasi na chanya. Wengi tunajua kwamba sehemu ya juu ya wingu huwa na chaji chanya na sehemu yake ya chini ni hasi. Kumbuka ardhi ina chaji chanya. Mgongano huu wa mawingu hutokea baada ya mawingu kupoteza hali yake ya utulivu kutokana na kuongezeka kwa joto la tabaka la chini kabisa la mawingu na unyevunyevu mwingi kutoka ardhini. Au mara chache hutokana na ongezeko la hali ya baridi katika tabaka la juu kabisa la mawingu. Ndio maana mara nyingi radi hutokea wakati wa mchana na mara chache sana wakati wa usiku. Na kwa sababu lazima kuwepo na unyevunyevu radi mara zote hutokea wakati mvua ikinyesha. Isipokuwa kwa wenzetu wa Sumbawanga ambao inasemekana radi hutokea pia wakati wa mchana kweupe, jua kali na hakuna mvua(ninatania lakini).

Chaji hizi  tofauti ni lazima ziwe kubwa kwa maana ya kiasi ili kuweza kupenya katika hewa kati yao na kuzalisha umeme. Hii ni kwa sababu hewa ina ukinzani mkubwa sana kwa umeme. Ikumbukwe kwamba mgongano mmoja tu kati ya mawingu unaweza kuzalisha umeme mwingi wa hadi milioni 100V.  Huu ni umeme mkubwa sana ukizingatia kwamba kwa matumizi ya nyumbani tunahitaji kiasi cha 220/230V. Mgongano huu huzalisha joto na mwanga mkali sana. Bahati nzuri ni kwamba huisha na kufifia mapema sana.

Kwa hiyo RADI ni UMEME. Ni umeme mkubwa unaoambatana na mwanga mkali na sauti kubwa sana. Kwa sababu ni umeme mkubwa, mara zote husababisha madhara makubwa sana kwa binadamu na mazingira yake. Madhara kwa binadamu ni pamoja na kifo au majeraha na hasara inayotokana na uharibifu wa mali. Lakini radi huharibu miundombinu ya umeme, mimea na nyumba pia. Kwa kiasi kikubwa madhara ya umeme yanaweza kuepukika kama kila mmoja ataelimishwa na kufuata taratibu za kujikinga na madhara yake. Kwa wenye majengo marefu wanahitaji kufunga kifaa kinachoitwa Lightening arrestor au thunderstorm arrestor. Katika majengo ya kawaida ni muhimu kuhakikisha Earthing System (Grounding) iko vizuri. Hakikisha wakati mvua inanyesha umevaa viatu au kandambili zenye soli pana kiasi cha kutosha. Ikiwezekana zima kabisa umeme unapoona dalili za radi, unaweza kuacha taa tu zinawaka ikiwa kutakuwa na giza wakati huo. Kamwe usisimame au kukaa katika maji au kusimama chini ya nguzo, mti mbichi au kitu chochote kinachokuzidi urefu na kina uwezo wa kupitisha umeme. Mara zote radi hutafuta njia fupi na rahisi ili kukamilisha muunganiko wake na ardhi.

Maeneo mengi ya vijijini watu wanapokutwa na mvua na hakuna sehemu ya kujikinga na mvua, hukimbilia chini ya miti. Ni hatari sana kufanya hivyo kwa sababu ikiwa mti uliosimama chini yake utakuwa ndio mrefu kuliko kitu kingine chochote kinachopitisha umeme mahali hapo, basi radi itakamilisha muunganiko wake na ardhi kupitia mti huo na hapo ndipo utakapokutana na balaa kubwa la kifo ama majeraha makubwa. Lakini pia kunapokuwa na dalili za radi jizuie kutembea kwa mwendo mrefu katika sehemu ya wazi sana ambayo wewe ndio utakuwa na kimo kirefu kuliko kitu kingine. Vinginevyo unaweza kuishia kuwa mkaa.

Wednesday, 2 November 2016

KWA NINI UMEME NI HATARI





Kuna sababu nyingi sana zinazonipa ujasiri wa kukutahadharisha na kukuambia umeme ni hatari. Ni hatari sana kwa maisha yako endapo tu hutazingatia kanuni zake. Hata hivyo hatuna namna ya kukwepa kutotumia umeme katika zama hizi za mageuzi makubwa ya teknolojia. Ukiweka pembeni madhara ya umeme kwa vifaa vinavyotumia umeme na mazingira kwa ujumla, umeme una madhara makubwa sana kwa mwili wa binadamu. Umeme huu tunaofurahia kuutumia una uwezo wa kuuunguza mwili, kujeruhi mishipa ya fahamu, kusababisha kifo au kuzimia.

 Wataalamu wa viumbe hai wanasema kwa kiasi kikubwa mwili wa binadamu umejawa na maji. Hali hii inasabaisha umeme kupita katika mwili wa binadamu bila kipingamizi kwa kiasi kikubwa. Madhara au majeraha yanayosababishwa na umeme katika mwili hutofautiana kutokana na udogo au wingi wa kiasi cha umeme uliopita hapo pamoja na urefu au ufupi wa muda umeme umepita katika mwili huo. Kiasi kidogo tu cha 1mA ambayo ni sawa na 0.001A kinaweza kumfanya mtu ajisikie vibaya na kuhisi maumivu kama vile anachomwachomwa na visindano vidogo vidogo.

 Hata hivyo, kadri kiwango cha umeme kinavyoongezeka ndivyo mshituko na maumivu makali yanavyoongezeka au kuwa makubwa katika mwili wa binadamu. Hali hii husababisha pia misuli kukakamaa na kuathiri viungo vingine vya mwili ikiwa ni pamoja na kuathiri utendaji kazi wa kawaida wa moyo na mapafu. Wakati mwingine nitakuelezea namna bora ya kujikinga na hatari za umeme.

BAADHI YA KAULI TATA KUHUSU UMEME

Hizo ni baadhi ya kauli tata kuhusu umeme. Ili kupata taarifa na habari zinazohusu Umeme endelea kujifunza kupitia blog hii ya Umeme na maisha.

Sunday, 30 October 2016

GESI NA UMEME KWA MAZINGIRA YETU





Kwa mujibu wa Tanzania D&H Survey, matumizi ya umeme mijini kwa aijli ya kupikia ni 3.8% na vijijini ni 0.2%. Wakati huo huo matumizi ya mkaa mijini kwa ajili ya kupikia ni 62% na vijijini ni 6.3%. Linapokuja suala la matumizi ya kuni hali ni mbaya zaidi kwa maeneo ya vijijini kwani watumiaji wa nishati hii inafikia 92% na mijini watumiaji wanafikia 21%.
Hizi ni takwimu za kuogopesha sana hasa kwa mazingira yetu na majaliwa ya vizazi vijavyo. Unaweza kupata picha halisi mwenyewe ni jinsi gani misitu yetu inateketea kila uchwao. Inasikitisha sana kwamba katika kila miti na misitu inayoteketetea kila mwaka ni robo yake tu ndio hupandwa tena baada ya matumizi ya ile ya awali. Hii inamaanisha misitu inazidi kuisha na itafikia wakati itabaki kuwa historia kama hatua madhubuti na za makusudi hazitachukuliwa.

Nia yangu ni kutaka kusisitiza nishati mbadala wa kuni na mkaa. Kwa wengi wetu matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia ni kama anasa kutokana na gharama kubwa ya umeme. Hata hivyo kuna nishati nyingine ya gesi ambayo wengi wetu bado hawajahamasika kabisa kuitumia. Nishati ya gesi ni rahisi sana kwa maana ya gharama kuliko hata mkaa kama utaamua kuzilinganisha. Pamoja na urahisi huo, gesi ina faida nyingi kwa mtumiaji kuliko nishati zingine zote nilizozitaja hapo juu. Jambo lingine la muhimu ni kwamba ukiondoa kuni na mkaa ambavyo vinasisitizwa kutotumiwa, usambazaji wa gesi ni rahisi sana kwa maeneo yote ya mijini na vijijini.

Hata hivyo kwa wakazi wa vijijini wana nafasi kubwa sana ya kuzalisha gesi yao wenyewe ukiachilia mbali hii gesi tunayouziwa na makampuni mbalimbali. Kuna gesi ya asili kabisa ambayo inazalishwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama na mabaki ya mimea mbalimbali. Teknolojia ya utengenezaji wa gesi hii ni rahisi na inapatikana kwa wataalamu kadhaa hapa nchini. Niliwataja wakazi wa vijijini kwa vile upatikanaji wa malighafi ya gesi hii ni mkubwa na rahisi sana vijijini. Kinachokosekana hapa ni uhamasishaji na mafunzo ya uzalishaji wa gesi ya aina hii. Kwa watu wa mijini ni vizuri wakahamasika kutumia gesi badala ya mkaa kama takwimu zinavyoonyesha hapo juu. Kufanya hivyo kutapunguza matumizi ya mkaa na kuni ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa sana kuharibu mazingira.

Ikiwa mazingira yetu yatatunzwa ipasavyo tutajihakikishia upatikanaji mzuri wa mvua ambayo itatuwezesha kuzalisha chakula cha kutosha na jambo jingine zuri ni kwa kampuni yetu ya kizalendo TANESCO kuweza kuzalisha umeme unaotokana na nguvu ya maji wa kutosha. Na hii ndio SABABU kubwa iliyonifanya leo hii nikaandika nilichokiandika. Kwamba tutunze mazingira yetu ili tupate mvua za kutosha na hivyo kuwawezesha TANESCO kuzalisha umeme wa kutosha. Hili linawezekana endapo sote kwa pamoja tutaguswa na uharibifu wa mazingira unaoendelea. Maana yake ni kwamba tubadili tabia na fikra zetu. Tufute fikra kwamba wanaoweza kutumia gesi ni matajiri tu. UKWELI ni kwamba gharama halisi za matumizi ya gesi ni ndogo kuliko gharama za kutumia mkaa. Siku nyingine MUNGU akinijaalia nitakuonesha ukweli huu kihalisia kabisa.

Sote tunafahamu kabisa kwamba TANESCO inazalisha umeme kutoka katika vyanzo kama gesi, maji na mafuta aina ya diesel kwa kiasi kidogo sana.  Kwa takwimu kutoka shirika la TANESCO, uzalishaji wa umeme kutokana na gesi ni 63% na maji ni 37%. Hata hivyo kuna uzalishaji kwa njia ya maji unategemewa kuanza muda mfupi ujao ambao utazalisha jumla ya 300MW. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha umeme kitakachozalishwa ukilinganisha na vituo vingine vinavyozalisha umeme kwa njia hii. Uzalishaji huu utaongeza kiwango cha asilimia hapo juu. Ninachotaka uone hapa ni jinsi ambavyo kama tukiyatunza mazingira yetu tunaweza kupandisha kiwango kikubwa zaidi cha uzalishaji umeme wa maji kuliko ilivyooneshwa hapo juu. Kwa hivyo, njia mojawapo ya kuyatunza mazingira ni kuhamasika kutumia gesi badala ya mkaa na kuni. Vile vile tuzalishe gesi inayotokana na mabaki ya mimea na kinyesi cha wanyama pale inapobidi/wezekana.

Pamoja na hayo yote niliyoyaeleza hapo juu, bado kuna nishati nyingine mbadala tuna nafasi ya kuzizalisha. Hapa namaanisha umeme unaozalishwa kutokana na jua na upepo. Umeme wa jua unaweza kuzalishwa katika maeneo yote nchi kwani upatikanaji wa jua ni wa uhakika. Hata katika maeneo yenye mvua nyingi, baridi kali na ukungu mwingi kama vile wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Njombe mkoani Njombe, Rungwe mkoani Mbeya bado uzalishaji wa umeme wa kutosha kwa matumizi ya nyumbani unawezekana. Kwa umeme unaozalishwa kutokana na upepo, tafiti zinaonesha maeneo ya Kititimo mkoani Singida na Makambako mkoani Njombe yana uwezo wa kuzalisha umeme mwingi kutokana na kasi ya upepo unaopatikana katika maeneo haya.

Wakati mwingine nitakuchambulia maeneo haya na kiasi cha umeme kinachoweza kuzalishwa. Kwa msaada wa taarifa zinazotolewa na TANESCO nitaainisha vituo vyote vinavyozalisha umeme wa gesi, maji na diesel na kiasi kinachozalishwa na vituo hivyo. Kisha tutafanya pamoja tathmini kadhaa za hali ya umeme na namna ambavyo tunaweza kuwashauri wazalishaji wa umeme namna tunavyoweza kuboresha na kuongeza upatikanaji wa umeme.